03/10/2025
Shirika la Jane Goodall Institute limethibitisha kwa huzuni kubwa kuwa mwasisi wake, Dkt. Jane Goodall, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91. Amefariki akiwa usingizini, huko Los Angeles, Marekani, alipokuwa kwenye ziara yake ya kutoa mihadhara.
Dkt. Goodall alikuwa mwanasayansi mashuhuri duniani kwa utafiti wake wa muda mrefu kuhusu sokwe mtu (chimpanzee). Mwaka 1960, alianzisha utafiti wa muda mrefu zaidi wa sokwe pori katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Kigoma, Tanzania, ambao unaendelea hadi leo.
Mbali na utafiti, alianzisha taasisi ya kimataifa ya Jane Goodall Institute, ambayo kwa zaidi ya miaka 40 imekuwa mstari wa mbele katika uhifadhi wa mazingira kwa kushirikiana na jamii. Pia alianzisha mpango wa kimataifa wa vijana wa mazingira uitwao 'Roots & Shoots', unaotekelezwa katika zaidi ya nchi 75 duniani.
Jane Goodall alikuwa balozi wa amani wa Umoja wa Mataifa, na kazi zake zimewasaidia watu wengi, hasa vijana, kujifunza, kuwa na matumaini na kujali mazingira. Dr. Goodall atakumbukwa k**a mmoja wa watu waliobadili kabisa namna dunia inavyowaelewa sokwe na maisha ya wanyama pori.